Mkuu wa chuo Cha Serikali za Mitaa LGTI
Dkt.Madale atembelea Banda la Chuo Sabasaba
Posted On: July 7th, 2022
Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dkt.Mpamila Madale ametembelea banda la maonesho la Chuo hicho kwenye maonesho ya 46 ya Biashara Sabasaba Jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuangalia jinsi Chuo hicho kinavyotoa huduma kwa wahitaji katika maonesho hayo.
Daktari Madale ametoa wito kwa wazazi, walezi pamoja na vijana wanaotaka kujiunga na Chuo hicho katika fani mbalimbali ikiwemo Maendeleo ya Jamii,Utawala katika Serikali za Mitaa,Uhasibu na Fedha,Utunzaji kumbukumbu na nyaraka,Ugavi na Manunuzi pamoja na Rasilimali kuanzia ngazi ya Astashahada ya msingi hadi Stashahada na wale wahitaji wa kujiunga na Shahada katika fani za Maendeleo ya Jamii,Utawala katika Serkali za Mitaa na Rasilimali watu kutembelea katika banda hilo lililopo katika banda la Jakaya Kikwete ili kupata wasaa mzuri zaidi wa kuuliza maswali mbalimbali na kujua kwa undani kuhusu Chuo cha Serikali za Mitaa.
Akiwa katika banda hilo pia Mkuu huyo wa Chuo alionekana akishirikishughuli mbalimbali za kutoa huduma kwa wageni waliokuja kutembelea katika banda hilo
“Kazi ya kuwahudumia wateja wetu ni ya kwetu wote bila kujali cheo ndio maana unaniona hapa na mimi natoa huduma kwa wateja waliokuja kupata huduma katika chuo chetu ikiwemo wanaohitaji kufanya udahili kwa njia ya mtandao na wale wanaokuja kuchukua fomu za kujiunga na Chuo baada ya kuchaguliwa na Serikali kujiunga na Chuo chetu” Alisema Dtk.Madale.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utawala na Fedha Dkt.Yusuph Mashala aliwataka watumishi wa chuo waliokuja kwa ajili ya maonesho hayo kuhakikisha wanajitahidi kutoa huduma bora katika kipindi chote cha maonesho kwani Chuo kinawategemea kukisemea vyema na pia akawataka wakipata nafasi kutembelea katika mabanda mbalimbali ili kujifunza mambo mazuri ya huko.
Chuo cha Serikali za Mitaa kinashiriki Maonesho hayo kwa lengo la kujitambulisha na kukitangaza Chuo pamoja na Programu zake na kufanya udahili wa kujiunga na Chuo hicho kwa Mwaka wa masomo 2022/2023.
Comments
Post a Comment